ARSENAL
KUFUTA UTEJA?
Na Abdul Rutona. (Msanifu wa Habari)
Kuelekea mtanange wa mahasimu
katika Ligi Kuu ya Uingereza hapa kesho kati ya Arsenal na Manchester United,
mengi yamesemwa na yanaendelea kusemwa hasa kwa washabiki wa timu hizo kubwa
mbili zilizo na idadi kubwa ya washabiki ulimwenguni kote.
Washabiki wa Arsenal wengi
wamekuwa na hamasa na kikosi chao cha mwaka huu wakichagizwa na kiwango kizuri
cha Alexis Sanchez na Danny Welbeck huku washabiki wachache
bado hawaamini kama kikosi chao cha mwaka huu ni imara.
Kwa upande wa Manchester United,
washabiki wa timu hii wengi hawafurahishwi na kiwango cha timu yao japo wana
wachezaji wenye kujitoa kama Wayne
Rooney na Angel Di Maria ila wachache bado wanaamini
kuwa pamoja na timu kutokuwa kizuri, vijana wa Wenger wataendelea kukaa kama kawaida. Dakika tisini za mchezo huo
ndizo zitakazoamua nani mbabe siku hiyo ya Jumamosi tarehe 22 – 11 – 2014 pale
kwenye uwanja wa Emirates utakaochezeshwa na Mwamuzi Mike Dean kama Mwamuzi wa Kati.
Katika kukutana na waandishi wa
habari, makocha walitoa mitazamo yao kuhusiana na mchezo huo na kutoa maendeleo
ya machezaji walio na majeruhi. Kwa upande wa Wenger alisema watu wasiangalie
nafasi za timu hizo katika msimamo bali waangalie uwezo wa wachezaji katika
timu hizo na kubashiri kuwa mechi itakuwa nzuri kwa kutazamwa. Kocha pia alitoa
habari za maendeleo za wachezaji waliokuwa na majeraha. Alisema mshambuliaji
wao Olivier Giroud amepona na
amekuwa akifanya vizuri hata kwenye mazoezi, pia nahodha wao Mikel Arteta naye anatarajia kuwepo.
Aliendelea kutoa taarifa kuwa mabeki Laurent
Korcielny, Mathieu Debuchy,
golikipa David Ospina na kiungo Abou Diaby wataendelea kutokuwepo. Pia Danny Welbeck aliyeonekana kuumia
katika timu ya taifa, ataangaliwa kama atawezacheza.
Kwa upande wa Machester United,
Kocha Van Gaal amesema kuwa
atawakosa Marcos Rojo, Phil Jones, Jonny Evans, Rafael na Falcao. Daley Blind pia natajiwa kukosa mchezo huo baada ya kuuumia kwenye
mechi kati ya timu yake ya Taifa ya Uholanzi ilipocheza na Latvia. Kwa upande
wa Luke Shaw, Angel Di Maria, Michael
Carrick na golikipa De Gea wanawezarudi
baada ya kupata matatizo madogo madogo.
Kuelekea mchezo huo, inaonesha
vijana wa Wenger wamekuwa kidogo
wanyonge wanapokutana na vijana wa Manchester United. Katika mechi 11
zilizopita, Arsenal wameshinda mechi moja, wametoa sare mechi tatu na kufungwa
mechi 7. Mara ya mwisho vijana hawa wa Wenger
kushinda ilikuwa mwaka 2011 kwa goli moja la Aaron Ramsey. Na mechi iliyoisha kwa magoli mengi ni ile ya Tarehe
28 – 08 – 2011 iliyomalizika kwa Arsenal kufungwa magoli manane kwa mawili.
Uwezekano wa wachezaji 11
watakaoanza:-
Historia itabaki
historia, rekodi hutengenezwa na huvunjwa.
KILA
LA KHERI.